Mkata wa maneno
Zacheka nami zangu chekeo
zacheka zafurahika
Sina mawazo kichwani leo
Bado hayajarauka ...
Nadhani ni asubuhi
imeanza kuchipuka
Nayo ndiyo sababu
ya moyo kuliwazika
na huu mdundo mtamu
mwema ulotandazika
Najichekea ... kwani najua vyema
kwamba sijazoea hali hii tabasama
ijitembezayo kwa shairi na kwa ngoma
ikichezacheza nami ... ikininyegeza kama mke na mume
kama wapenzi daima
Najua sijaizoea hali hii ya furaha na shauku
ijigambayo kwa mchana na usiku
kufuata mtindo wa manju kila siku
... kufuata anasa za dunia
Ndipo nikawa mkata...
mkata wa maneno ya furaha na amani
ya mahaba au dini
maneno ya kufifisha kisasi cha mja
juu ya maisha duniani
maneno ya kushinda vita vya nyoyoni
hivyo vita vya ndani kwa ndani.
Neno langu ni maumivu tu, ni mashaka
Ndipo kapendelea mwenendo wa kale ...
fikira kutoziandika.