Poems

Jumapili ya Damu

 
Midundo ya Reggae
Inarindima hewani
Na kuchanganyika
Na macheo
 
Katika jiji
Vioo, madirisha
Na milango
Inasalimu amri
Kutoka kumbo kali
Za wenye njaa
Na matarajio
Ya miongo miwili.
 
Ndani ya maduka
Mawimbi ya watu
Yanapaa, kushuka
Na kupanda kwingineko
Huku rafu na kuta
Zikibadilika sura
Kama tanzu za miti
Kiangazi kinapojiri.
 
Vifaa vya kila ukoo
Nguo za kila rangi
Zinaketi vichwani
Kuninginia mikononi
Kulala migongoni
Au kubanwa kwapani
Zikibadili makazi
Na umiliki.
 
II
 
Risasi
Zinaanza kupiga miluzi
Na kwa ghadhabu
Kushtua kuta
Milingoti ya stima
Magari ya rangirangi
Na nyama na mifupa
 
Watu wanaterereka
Damu inatiririka
Uhai unaporomoka
 
III
 
Ghafla
Midundo ya Reggae
Inakauka
Na nyimbo za jana
Kurudi angani
Kama uvundo ambao
Umevamia pua tena
Baada ya kuangushwa
Na kumbo la upepo
 
Kutoka mwangu jikoni
Barabara ni dhahiri-
Magari ya rangirangi
Vifaru vya madoadoa
Vinatiririka kama mto,
Bunduki zinalenga kushoto
Kulia, nyuma na mbele
Nayo mizinga hatari
Inatega mbingu;
Huu mtiririko
Ni safari ya marejeo
Anarejea mungu-wa-kinamo
Kwenye ulingo.
 
IV
 
Katika fahamu
Mawazo mbalimbali
Yanapita kwa zamu
Kama vipepeo na nondo
Wakipita kwa makundi
Mbele ya macho;
Kwa tabasamu
Nakumbuka Obasanjo
Na uamuzi wake angavu
Bali pia
Kwa huzuni
Nakumbuka Bokassa na Amin,
Na Mobutu na Doe,
Na damu na mafuvu
Matita ya mafuvu!
Magurudumu ya mawazo
Yanafikia njia panda
Na kwa muda, kukwama
Kabla ya kuanza safari tena
Kwenye njia wazi
Ya serikali ya kiraia
 
Hata inapoongozwa
Na genge la mazimwi