Poems

Chai ya Jioni

Wakati tunywapo chai hapa upenuni
Na kuwatazama watoto wetu
Wakicheza bembea kwa furaha
Tujue kamba ya bembea yetu
Imeshalika na imeanza kuoza
Na bado kidogo tutaporomoka.
 
Kulikuwa na wakati ulinisukuma juu
Nikaenda zaidi ya nusu duara;
Kulikuwa na wakati nilikudaka
Ulipokaribia kuanguka,
Na kulikuwa na wakati tulibebana kwa zamu
Mmoja wima akisukuma mwingine amekaa.
Wakati huo, japo tulipaa mbele na nyuma
Tulicheka kwa matumaini yaliyotiwa chumvi
Na kisha tukaongozana jikoni kupika chajio;
Ilikuwa adhuhuri yetu.
 
Sasa tukisubiri ndoto tusizoweza kutekeleza tena
Tumalizie machicha ya chai yetu ya jioni
Bila kutematema na kwa tabasamu.
Baada ya hapo tujilambelambe utamuutamu
Uliobakia kwenye midomo yetu,
Tukikumbuka siku ilee ya kwanza
Tulipokutana jioni chini ya mwembe
Tukitafuta tawi zuri gumu
La kufunga bembea yetu
Naye mbwa Simba akikusubiri.
 
Lakini kabla hatujaondoka kimyakimya
Kukamilika nusu duara iliyobakia.
Tuhakikishe vikombe vyetu ni safi.