Poems

Nilivuka

Nimevuka mabara kuja Afrika
Lakini siku katu haikufika
            ya milima kuwa vilima
            ya mito kuwa vijito
            vya kuweza kudakiika.
Sijakufikia mpenzi
kama kwamba u nyota ya mbali
kama kwamba umemea baina yetu
            ukuta wa usingizi.
Nikikushika, mikono huwa haishiki
ila maiti ilokufa bila haki
            kama kukumbatia damu yangu jiweni
            katika nyumba iloghariki kwa tufani
            ambayo usiku wake umesimama makini
            na asubuhi yake imekwama mbali
                                                                        ikisubiri njiani.
 
Miaka imenyumbuka baina yetu: damu na moto,
Daraja nikazikwea zilogeuka ukuta
Na wewe, ukazama chini baharini
                                                            nisiweze kukugusa.
Mashaza yakanichuna, yakikata mishipa
                                                            ya mikono yangu,
Nami nikaita:
            Ewe Afrika
            mpenzi wa roho yangu,
            mwenzi wa mabuu na giza,
            Nimezunguka miaka mingi kukutafuta
            na safari yangu bado haijakatika
            ewe maiti ulojifinika kwa yako maisha.
 
Nimevuka mabara kuja Afrika
lakini siku katu haikufika
ya daraja kuweza kuvukika.
Ewe ulalaye nami kitandani
U kama nyota ya mbali mbinguni
ulo milango ilofungwa kwa ndani
Nami nimesimama nje
                                    nasubiri baridini.