Poems

Kisima

Kisima cha maji ya uzima ki wazi
Na vyura katika bonde la taaluma watuita
Tujongee kwa mahadhi yao
Yaongozayo pandikizi la mtu
Kwa hatua ndefu litembealo
Na sindano ya shaba kitovuni
Upinde na mishale mkononi
Kisha likapiga goti kisimani
Tayari kumfuma akaribiaye
Maana shujaa hafi miongoni mwa wezi
Bali kama simba mawindoni.

Hatuwezi tena kuteka maji
Na kalamu zetu zimekauka wino.
Nani atamsukuma kwa kalamu
Aitwe shujaa wa uwongo!
Aliyeitia kitovuni kwa hofu
Ingawa tegemeo hakulipata
Alifungua mlango uelekeao
Katikati ya ujuzi na urazini mpya
Mwanzo wa kizazi tukionacho.

Share this poem