Poems

Ewe bibi mwenye enzi

Ewe bibi mwenye enzi, salamu zangu pokea
Mbona unanipa kazi, pendo sijalizowea
Roho ina majonzi, moyo umejiinamia
Fikiri utanabahi, pendo lipi ni la kweli
 
Ulisema wewe wangu, Mpaka mwisho wa dunia
Ukaapa jina la mungu, hutobadili nia
Sasa kama si mwenzangu, mbona unanikimbia
Fikiri utanabahi, pendo lipi ni la kweli
 
Siku tuliyoonana, leo naikumbukia
Jinsi tulivyopendana, kwangu ukizingatia
Leo mbona twatupana, hukufika nusu njia
Fikiri utanabahi, pendo lipi ni la kweli
 
Niko mbele ya kaumu, haya zimeniingia
Moyo unanilaumu, pendo lako kuridhia
Mpenzi sijafahamu, nini umekusudia
Fikiri utanabahi, pendo lipi ni la kweli